Ali—“Sifa ni kipimo cha ustahili wa watu. Mtu hawezi kuwa na ustahili kama hana sifa.”
Idi—“Kama sifa ni kipimo cha ustahili, kumbuka na kufahamu kwamba kipimo chenyewe si madhubuti. Watu wengi wana sifa lakini hawana ustahili; na wengine wana ustahili lakini hawana sifa.”
Ali—“Wakusudia kusema kwamba watu wasio thamani au ustahili hupata sifa kwa sababu ya kujipendekeza kwa kushawishi huba za watu? “
Idi—“Naam, hiyo ndiyo shabaha yangu. Watu wasifuo watu fulani, nao husifiwa vile vile. Kwa hivi hupata sifa bila kuwa na ustahili wowote. Watu wengi hawana akili; hufuata wengine kama vipofu. Hawana wakati wala maarifa ya kupimia ustahili wa wengine. Watu wasio na ustahili hupata sifa mara kwa mara kwa kujitangaza. Pengine, hata magazeti husifu watu wasio na maana.”
Ali—“Nasikia usemayo, lakini sifahamu bado kwa nini ustahili udaio kuwa bora hushindwa mara nyingi kupata sifa?”
Idi—“Kwa kuwa ustahili una ubora wa nafsi, watu walio nao hawijidunishi kwa kujipendekeza kwa watu. Hawarairai wengine wala hawajitangazi makusudi wapate sifa. Wana ari kubwa katika mioyo yao. Johari nyingi zenye nuru bora hujificha gizani, lakini hazififii milele.”
Ali—“Naona vigumu kusadiki kwamba vitu vingi vipatavyo sifa havina thamani wala ustahili wowote. Kwa desturi, watu hawasifu kitu bure hata kama ni wajinga kama nini.”
Idi—“Vitu visivyo thamani vikitangazwa vema, watu huona vina ustahili ambao kwa kweli hauonekani ndani yake. Vitabu, madawa na sanaa zisizo maana hupata sifa. Mwandishi, mshairi au mwimbaji ajidunishaye makusudi kuridhisha ulafi wa watu, husifiwa. Hadithi chafu ya kusisimua damu kwa uuaji, pepo na mazimwi hupata sifa bora kuliko Al-Inkishafi, Diwani ya Muyaka au Mwana Kupona.
“Wasanifu wasio maana husifiwa kwa sababu huwapa watu watakacho. Msanifu hasa hawapi watu watakacho. Jicho lake halitazami sifa. Hutazama adili na usanifu bora. Pana methali inenayo ‘ Watu bora hawasifiwi katika nyakati zao.’ Hili huonyesha kwamba watu wengine hawajali sifa. Huongozwa na bidii na hamu katika matendo yao.”
Ali—“Walakini, mimi naona kwamba sifa na ustahili kama kitu kimoja. Watu wapenda sifa kama wapendavyo ustahili. Ustahili usio sifa hauna maisha.”