1. Wajibu wa utu wema
2. Utu wema ni nini?
3. Utu wema hulelewaje?
4. Manufaa ya utu wema
Utu wema ni rai, duniani kila pembe,
Ubaya ni uadui, huchukiza kwa viumbe.
Katika dunia hii iliyojaa mashaka, tusiongezeane huzuni juu ya huzuni kila siku kwa matendo yetu ya ukatili. Badala yake tungetia furaha katika maisha yetu kwa utu wema. Maneno mema hayagharimu zaidi kuliko maneno mabaya. Basi kwa nini hatutumii maneno mema?
Mtu mwenye utu wema ni mstahifu, mpole, mtulivu, mwema, karimu na mcheshi. Mwema kwa wote—maskini na tajiri, kijana au mzee, watumishi au mabwana. Hata akiwa katika mashaka, tabia yake ni ile ile. Hapotelewi na uzuri wa utu wema wake asumbuliwapo na wengine.
Kwa desturi utu wema twazaliwa nao. Afya, utajiri, na matendo mema huweza kusitawisha utu wema wetu, lakini tukipotolewa toka kuzaliwa, mambo haya hayawezi kutufanya watu wema. Elimu huweza kusitawisha tabia zetu, lakini haiwezi kuleta utu wema. Katika kulea mmea mwororo wa utu wema, mama ana sehemu kubwa ya kazi. Watu wengine huwa na tabia mbaya kwa sababu ya kusumbuliwa na mama zao. Pengine hata mtu mwema huwa mbaya asumbuliwapo na ugonjwa, umaskini, matukano na utovu wa shukrani wa wengine.
Utu bora hutumika kama stashahada ya maendeleo. Utakufungulia milango ya kukutana na watu bora. Kila mtu atakupenda tena atakusaidia. Katika kila njia ya maisha ambayo utakuwamo, utapata msaada na faraja. Wema wako utatuzwa kwa wema, maana, kwendako mwinyi hurudi mwinyi. Hili litafurahisha maisha yako nawe utaridhika. Kinyume chake ni kwamba tabia mbaya za watu wengine hupinga sana maendeleo yao.
Utu wema ni johari kubwa kwa watu. Ukitupa changarawe katika maji, hufanya viwimbi vingi ndani yake. Kwa njia hii hii kabisa, utu wema wako hufanya viwimbi vingi vya wema katika mioyo ya watu. Maneno mema huleta matendo mema. Neno jema hutuliza hasira, kama maji yazimavyo ukali wa moto. Au kama methali isemavyo, “Neno jema hutoa nyoka pangoni.” Ucheshi wako utaenea kila pahali kama nuru ya jua. Adabu au wema wako kwa mtu utamfanya awe na adabu au mwema kwako. Kwa njia hii wema utaenea kwa watu. Kinyume chake ni kwamba tabia mbaya husumisha chemchemi ya furaha.